Pastor | Former Member of parliament-iringa constituency 2010 -2020 | Former Shadow Minster for Natural Resource and Tourism 🇹🇿

Iringa, Tanzania
National security inageuka kuwa regime security pale ambapo taasisi zilizoundwa kulinda taifa zinaanza kutafsiri usalama wa walioko madarakani kuwa sawa na usalama wa taifa. Tofauti hiyo inaweza kuonekana kwa vipimo hivi: 1. Ukosoaji unapogeuzwa kuwa tishio la kiusalama. Mwananchi anayemkosoa Rais, Serikali au chama tawala anaanza kutazamwa si kama mkosoaji wa kisiasa bali kama mtu anayehatarisha taifa. 2. Upinzani unapogeuzwa kuwa adui wa dola. Kushindana na chama tawala, kutaka kukiondoa kupitia uchaguzi au kudai mabadiliko ya Serikali kunaanza kutafsiriwa kama kuhatarisha nchi. 3. Vyombo vya usalama vinapoanza kulinda political survival ya watawala. Badala ya kuuliza “Tanzania iko salama?” mfumo unaanza kuuliza “Serikali hii itaendelea kuwa madarakani?” 4. Sheria za usalama zinapotumika kusimamia migogoro ya kawaida ya kisiasa. Masuala yanayopaswa kujibiwa kwa hoja, uchaguzi, Mahakama au siasa yanaanza kushughulikiwa kama masuala ya usalama wa taifa. 5. Maslahi ya chama yanapochanganywa na maslahi ya taifa. Hapo kumpinga chama tawala kunaanza kuonekana sawa na kuipinga nchi. 6. Kulinda kiongozi kunapokuwa muhimu kuliko kulinda taasisi. Rais au Serikali inaanza kulindwa dhidi ya accountability badala ya Urais na Serikali kulindwa kwa kuhakikisha zinafanya kazi ndani ya Katiba. 7. Taifa linapoanza kuogopa mabadiliko halali ya madaraka. Uchaguzi unaanza kutazamwa kama salama ikiwa chama tawala kinashinda, lakini uwezekano wa kushindwa kwake unaonekana kama instability au security threat. Kipimo rahisi kabisa ni hiki: National security hulinda mfumo ambao unaweza kubadilisha watawala. Regime security hulinda watawala dhidi ya mfumo unaoweza kuwabadilisha. Kwa hiyo national security yenye afya inaweza kuilinda Serikali dhidi ya mapinduzi, ugaidi au uvamizi—lakini wakati huohuo ilinde haki ya wananchi kuiondoa Serikali hiyo kwa kura. Siku vyombo vinapoanza kuona kupoteza madaraka kwa watawala kama kupoteza usalama wa taifa, hapo mstari umevukwa: national security imeanza kuwa regime security.
5
50
152
3,759
Hongera sana Bunda
3
19
217
3,271
“Ukimya wa wenye uwezo wa kusema unaweza kuwa na athari kubwa kuliko makosa ya wenye mamlaka. Mamlaka yanaweza kufanya kosa mara moja; lakini ukimya wa wasomi, viongozi wa dini, wanahabari na raia wenye ushawishi hulifanya kosa hilo kuwa la kawaida, kulipa uhalali na kulifanya lirudiwe tena na tena.” Rev. Peter Simon Msigwa
4
22
69
1,957
MNAKERWA NA WIMBO WA JOEL NA DIAMOND? Rev. Peter Simon Msigwa Nimeona Wakristo wengi wakimlaumu Joel kwa kuimba pamoja na Diamond. Lakini wengi ninaowaona wakipaza sauti katika jambo hili, sijawasikia wakipaza sauti kuhusu mauaji ya tarehe 29/10/2025, rushwa, wizi wa kura, kutekwa na kupotea kwa watu, ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu. Ninajiuliza: Kwa nini tuna ujasiri mkubwa wa kumkemea mwimbaji, lakini tunakosa ujasiri huo huo mbele ya wenye mamlaka? Mungu anayesema “Usiue” ndiye anayesema “Usiibe” (Kutoka 20:13, 15). Utakatifu wake hauishii kwenye nyimbo na majukwaa ya muziki. Unagusa pia namna tunavyotumia mamlaka, tunavyowatendea wanyonge na tunavyosimamia haki. Katika Mika 6:8, Mungu anaweka wazi anachokitaka kwa mwanadamu: kutenda haki, kupenda rehema na kwenda kwa unyenyekevu pamoja naye. Hatuwezi kudai tunatembea na Mungu huku tukipuuza haki na rehema anazotutaka tuishi. Na hata tunapotumia 2 Wakorintho 6:14, kuhusu kutofungwa nira pamoja na wasioamini, tunapaswa kulitafsiri kwa uaminifu. Hatupaswi kulifanya kuwa marufuku ya kila aina ya ushirikiano na mtu asiyeamini. Katika 1 Wakorintho 5:9–10, Paulo anaeleza kwamba hakumaanisha waamini wajitenge kabisa na watu wa dunia; kufanya hivyo kungewahitaji kutoka duniani. Tunahitaji kuchunguza maudhui ya wimbo na aina ya ushirikiano wenyewe kabla ya kutoa hukumu. Lakini hata kama mtu anaamini Joel amekosea, hilo haliondoi wajibu wake wa kukemea dhuluma nyingine. Huwezi kujifanya mlinzi wa utakatifu kwenye jukwaa la muziki, huku ukitetea ukimya mbele ya damu ya binadamu. Yesu alilikemea hili katika Mathayo 23:23–24. Aliwakemea viongozi wa dini waliokuwa makini katika mambo madogo huku wakiacha mambo makuu ya sheria: haki, rehema na imani. Akawafananisha na wanaochuja mbu lakini wakameza ngamia. Yesu hakuwataka waache wajibu mmoja ili watimize mwingine. Aliwataka wayatende hayo bila kuyaacha yale mengine. Je, nasi tunachuja majukwaa ya waimbaji, huku tukimeza dhuluma za wenye mamlaka? Tatizo si kumhoji Joel. Tatizo ni kuwa na viwango viwili: ukali kwa asiye na mamlaka na upole kwa mwenye mamlaka; kelele kuhusu mwimbaji na ukimya kuhusu wanaodhulumiwa. Katika Yakobo 2:1–9, waamini wanaonywa dhidi ya upendeleo unaompa mwenye hadhi heshima huku ukimdharau maskini. Imani yetu haipaswi kubadilisha kipimo cha ukweli kwa kuangalia cheo, mali au ushawishi wa tunayemkemea. Kanisa linapaswa kujiuliza: Tunatetea kweli ya Mungu, au tunachagua ukweli ambao hautatugharimu urafiki, nafasi na upendeleo? Mithali 31:8–9 inatuelekeza kufungua vinywa vyetu kwa ajili ya wasioweza kujitetea, kuhukumu kwa haki na kutetea wanyonge na wahitaji. Wajibu wetu hauishii katika kusema nani hapaswi kuimba na nani. Unahusisha pia kusimama na wale ambao sauti zao zimezimwa. Na katika Isaya 1:15–17, Mungu anakataa ibada inayokwenda sambamba na mikono iliyojaa damu. Anawaita watu waache uovu, wajifunze kutenda mema, watafute haki na wawatetee wanaodhulumiwa. Mungu tunayemwimbia anajali pia watu tunaowanyamazia wanapodhulumiwa. Imani inayokemea pale palipo salama tu, lakini ikanyamaza pale penye gharama, inahitaji kujichunguza. Mungu habadilishi viwango vyake kulingana na cheo cha mtenda dhambi. Tusimtumie Mungu kuhalalisha hofu zetu. Kama tunasimamia utakatifu, tusimamie pia haki, utu na uhai wa mwanadamu. TUSICHAGUE DHAMBI ZA KUKEMEA KWA KUANGALIA NANI AMEZITENDA.
21
38
207
11,087
“If you can’t die for something you’re not worthy living “ Asante sana Mwenyekiti wetu!
3
42
191
2,839
Kwa mujibu wa Paul Chacha hawa ni Mali ya CCM! Watoke hadharani wajibu hilo iambo!
48
97
584
12,394
Hii ndio thinking ya viongozi wa ccm na ni hatari sana kwa usalama wa Taifa . Hapa ndio unaona umhimu wa madai ya Chadema No reforms no election! Maneno haya ni hatari kwa usalama wa Taifa! Serikali inaundwa kwa kufuata katiba ya CCM ?
62
118
497
86,887
CCM SI MFADHILI WA WATANZANIA Joseph Ki-Zerbo aliweka msingi muhimu wa kuelewa maendeleo aliposema: “Huwezi kuwaendeleza watu; watu wanajiendeleza wenyewe.” Maana yake si kwamba Serikali haina wajibu. Maana yake ni kwamba wananchi wenyewe ndio wahusika wakuu wa maendeleo yao. Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira yanayowezesha maarifa, kazi, ubunifu na juhudi zao kuzaa matunda. Kwa hiyo, CCM haiwezi kujiweka kama mfadhili wa Watanzania. Wananchi si wapokeaji wa hisani ya chama; ni wenye nchi, walipa kodi na wenye haki. Mkulima analima, mfanyabiashara anatafuta masoko, mfanyakazi anatoa huduma na kijana anahangaika kutengeneza ajira. Swali ni hili: Sera na utendaji wa Serikali vinawasaidia kusonga mbele au vinawawekea vikwazo? Mwananchi anayefanya kazi kwa bidii lakini akazuiwa na urasimu, akakosa soko la uhakika, akakosa elimu bora au akanyimwa haki, hahitaji kuambiwa avumilie na kukishangilia chama. Anahitaji Serikali inayotatua matatizo hayo. Hata mwanachama wa CCM anayepambana na umaskini hawezi kula uanachama, kulipa ada kwa kauli mbiu, wala kutibu mtoto kwa kushangilia viongozi. Anahitaji kipato, huduma bora na nafasi ya kutumia uwezo wake kujenga maisha yenye heshima. Kadi ya chama si njia ya kutoka kwenye umaskini. Mazingira yanayowezesha juhudi za wananchi kuzaa matunda ndiyo msingi wa maendeleo. CCM, kama chama kinachoongoza Serikali, inapaswa kujibu: Mmeunda mazingira gani yanayomwezesha Mtanzania kujikwamua kwa juhudi zake? Pale sera au utendaji wa Serikali vinapokwamisha juhudi hizo, nani anawajibika? Barabara, shule na hospitali zinazojengwa kwa fedha za umma si zawadi kutoka kwa chama. Ni utekelezaji wa wajibu wa Serikali kwa wananchi. Wananchi wana haki ya kuhoji ubora wake, gharama zake na namna zinavyowanufaisha bila kudaiwa shukrani za kisiasa. Wananchi hawana deni la utii kwa chama kwa sababu Serikali imetimiza wajibu wake. Serikali ndiyo yenye wajibu wa kuwajibika kwa wananchi. Huwezi kuwaendeleza watu kwa kuwanyamazisha, kuwafanyia kila uamuzi na kuwafanya wajione hawana uwezo bila chama. Wawezeshe kwa elimu, linda haki zao, sikiliza mawazo yao na waondolee vikwazo vya kutumia uwezo wao. Watanzania hawahitaji chama kinachojifanya mmiliki wa maendeleo yao. Wanahitaji Serikali inayowawezesha kujiendeleza wenyewe.
1
17
46
1,318
MWIZI WA KAWAIDA NA MWIZI WA KISIASA Rev. Peter Simon Msigwa Kuna tofauti gani kati ya mwizi wa kawaida na mwizi wa kisiasa? Mwizi wa kawaida anaiba pesa zako, simu yako, begi lako, saa yako au vito vyako. Hasara yake unaiona: mfuko uko wazi, simu haipo, pesa zimepotea. Lakini mwizi wa kisiasa anaweza kukuibia bila kuingia nyumbani kwako. Anaweza kutumia mamlaka uliyomkabidhi kuharibu maisha yako na ya watu ambao hata hawajazaliwa. Fedha za shule zinapoibwa, kinachopotea si fedha peke yake; ni nafasi ya mtoto kupata elimu bora. Fedha za hospitali zinapoliwa, kinachopotea si tarakimu kwenye hesabu; ni dawa, vifaa na nafasi ya mgonjwa kupona. Rasilimali za umma zinapogeuzwa mali ya wachache, kinachopotea ni ajira, huduma, fursa na matumaini ya wananchi. Mwizi wa kawaida anaiba ulicho nacho. Mwizi wa kisiasa anaweza kuiba hata nafasi yako ya kupata usicho nacho. Hapo ndipo uzito wa wizi wa kisiasa ulipo. Madhara yake yanaweza kuendelea muda mrefu baada ya mwizi kuondoka madarakani. Lakini kuna tofauti nyingine inayotupasa kutushtua. Mwizi wa kawaida haji kukuomba ridhaa ya kukuibia. Hakuombi umpatie dhamana. Hakuahidi kwamba atalinda mali yako. Mwanasiasa anakuja kwa ahadi. Anaomba umwamini. Anaomba umchague. Anaahidi kulinda maslahi yako, kusimamia mali ya umma na kutumikia wananchi. Anapotumia nafasi hiyo kujinufaisha, anakuwa amevunja zaidi ya wajibu wake: ameisaliti imani ya watu waliomkabidhi mamlaka. Hata hivyo, wananchi hawapaswi kulaumiwa kwa kila usaliti wa viongozi. Wengine hudanganywa kwa ahadi; wengine hukosa taarifa; wengine huishi katika mazingira ambamo uchaguzi na uhuru wa kuhoji vinawekewa vikwazo. Lakini pale tunapopata nafasi ya kufikiri, kuuliza na kufuatilia, hatupaswi kuikabidhi akili yetu kwa chama wala dhamiri yetu kwa kiongozi. Kupiga kura hakumalizi wajibu wa mwananchi. Kunaanzisha wajibu wa kufuatilia dhamana aliyotoa. Sasa fikiria jambo hili. Tunapohofia mwizi wa kawaida, tunafunga milango, tunaweka kufuli na tunaimarisha ulinzi. Tukimkamata, tunataka sheria ichukue mkondo wake. Lakini katika siasa, wakati mwingine tunawalinda wale tunaopaswa kuwahoji. Tunagombana na majirani zetu. Tunavunja urafiki. Tunagawanyika katika familia. Tunawatukana wanaouliza fedha za umma zimetumikaje. Mtu anauliza, “Fedha za hospitali zimekwenda wapi?” Tunamjibu, “Unakichukia chama chetu!” Mtu anauliza, “Kwa nini ahadi haijatekelezwa?” Tunamwita adui. Swali kuhusu fedha linageuzwa kuwa ugomvi kuhusu uaminifu. Mwenye kuuliza anakuwa mshtakiwa, na mwenye dhamana anapona kujibu! Hapo tunapaswa kujiuliza: tunalinda nini hasa? Jina la kiongozi au maisha ya wananchi? Sifa ya chama au mustakabali wa watoto wetu? Kama tunakasirishwa zaidi na anayeuliza kuhusu ubadhirifu kuliko ubadhirifu wenyewe, tunahitaji kuchunguza uaminifu wetu. Na kama tabia tunayoikemea kwa mpinzani tunaishangilia inapofanywa na mtu wa chama chetu, hatuna kipimo cha haki. Tuna kipimo cha upendeleo. Mwanasiasa ni mtumishi mwenye dhamana. Mamlaka aliyonayo yanatoka kwa wananchi na yanapaswa kutumika kwa manufaa yao. Kwa hiyo, kuhoji matumizi ya mamlaka ni wajibu wa uraia. Kudai hesabu ni kulinda mali ya umma. Kutaka uwajibikaji ni kuheshimu uzito wa nafasi ya uongozi. Uungwaji mkono haupaswi kuwa kinga dhidi ya maswali. Tunaweza kusema kwa uwazi: “Tutakuunga mkono unapofanya vizuri. Utakapokosea, tutakukosoa. Tutakapohitaji majibu, tutakuuliza. Na ukivunja dhamana, tutadai uwajibike.” Huo ndio uaminifu unaoilinda nchi. Pia, tuhuma za wizi zinapaswa kuchunguzwa kwa ushahidi na kwa haki. Uwajibikaji una nguvu pale ambapo sheria inatumika kwa wote, bila kuchagua upande wa kisiasa. Tusikubali chama kiwe mahali pa kuficha makosa. Tusikubali urafiki uwe sababu ya kunyamazia matumizi mabaya ya mamlaka. Tusikubali watoto wetu warithi gharama ya ukimya wetu. Mwizi wa kawaida anaweza kukuibia leo. Mwizi wa kisiasa anaweza kuweka mazingira yatakayowafanya watoto wako walipe kesho.
2
17
43
2,850
Nooo hapa ana mislead lazima tuweke mambo sawa , swala la Lissu hawana ujanja
Replying to @MsigwaPeter
Huyu mtu anatafuta tension nanyi msivyoona mbele mnajadili mnampa Airtime ya bure badala ya kuuzwa,sio kila JAMBO unahitaji kulitolea ufafanuzi---' anajaribu kuwatoa kwenye focus ya kesi ya mwenyekiti wetu huyu mtu hasipewe tension yoyote... mjadala hapa ni lissu
1
2
16
3,972
KANISA HALIHITAJI RUHUSA YA MAMLAKA KUSEMA UKWELI Rev. Peter Simon Msigwa Makonda, Kanisa si Serikali, lakini Kanisa ni sehemu ya jamii. Watu wanaoketi kanisani Jumapili ndio wanaokutana na hali halisi ya maisha Jumatatu. Maumivu yao hayaishii mlangoni mwa kanisa, wala wajibu wa mchungaji hauishii mimbarini. Kanisa likiona dhuluma, lina wajibu wa kusema. Likiona uongo na matumizi mabaya ya mamlaka, lina wajibu wa kukemea. Wananchi wanapoteseka, lina wajibu wa kusikia kilio chao na kusimama nao. Serikali inapofanya mema, lina sababu ya kuyatambua na kuyapongeza. Kipimo cha Kanisa kinapaswa kuwa ukweli na haki, si furaha au hasira ya mwenye mamlaka. Kumtetea anayedhulumiwa hakuligeuzi Kanisa kuwa chama cha upinzani. Kuonya mwenye mamlaka hakumfanyi mchungaji kuwa adui wa Serikali. Na kuombea viongozi hakumaanishi kuhalalisha kila wanachofanya. Biblia inatufundisha kuwaombea wenye mamlaka. Pia inatuonyesha watumishi wa Mungu waliowaonya wenye mamlaka walipokosea. Nathani alimkabili Daudi. Hakuficha kosa la mfalme nyuma ya heshima ya kiti chake. Yohana Mbatizaji alimkemea Herode. Hakupima ukweli kwa usalama wake binafsi. Mikaia alikataa kuungana na manabii waliomwambia Ahabu kile alichotaka kusikia. Wingi wa waliomsifia mfalme haukuufanya uongo wao kuwa ukweli. Kwa hiyo, hatuwezi kuwaheshimu manabii wa Biblia kwa ujasiri wao, halafu tukawataka watumishi wa leo wakae kimya wanapoona maovu. Hatuwezi kumpigia makofi Nathani wa jana huku tukimnyamazisha Nathani wa leo. Makonda, tunahitaji kutofautisha kuheshimu mamlaka na kuabudu mamlaka. Heshima haifuti uwajibikaji. Cheo hakimpi mtu ukiritimba wa ukweli. Na mamlaka ya mwanadamu hayawezi kuwa kipimo cha mwisho cha mema na mabaya. Iwapo hoja ni kwamba Kanisa lisikosoe Serikali, basi swali ni hili: Serikali inapongeza sauti za viongozi wa dini wanaoisifia, kwa nini isisikilize pia sauti zao wanapoionya? Kanisa haliwezi kukubalika linapotoa baraka, halafu likakataliwa linapokumbusha wajibu. Kiongozi anayekubali maombi ya mchungaji anapaswa pia kuwa tayari kutafakari maonyo yake. Maombi na maonyo yote yanaweza kutoka katika dhamiri inayomtaka afanikiwe kwa kutenda haki. Na hapa Kanisa lenyewe lina wajibu mkubwa: liseme kwa ushahidi, lisieneze uongo, lisichochee chuki, wala lisifiche upendeleo wa kichama nyuma ya jina la Mungu. Liwe tayari kukemea kosa hata linapofanywa na mtu anayelipenda, anayelisaidia au anayelikubali. Uaminifu wa Kanisa hupimwa pia kwa uwezo wake wa kuwaonya marafiki zake. Huwi dhaifu kwa kuonywa. Unapata nafasi ya kuona jambo ambalo wapambe wanaweza kuwa wanakuficha. Hatari ya kuzungukwa na watu wanaokubali kila unachosema ni kwamba, baada ya muda, unaweza kuanza kuamini kuwa huwezi kukosea. Makofi yanaweza kufunika kilio cha wananchi masikioni mwa kiongozi. Hayafuti maumivu yao. Ndiyo maana mamlaka yanahitaji sauti huru; watu wanaoweza kusema, “Hapa mmekosea,” bila kupimwa kwanza uaminifu wao kwa chama au ukaribu wao na watawala. Kanisa lisigeuke kuwa idara ya Serikali. Mimbari isigeuke kuwa majukwaa ya kuhalalisha kila uamuzi wa wenye vyeo. Dhamiri ya mchungaji isifungwe na zawadi, ukaribu na viongozi au hofu ya kupoteza mwaliko kwenye hafla. Mwananchi anayelia anahitaji zaidi ya kuambiwa avumilie. Anahitaji kuona kwamba hata mwenye mamlaka anakumbushwa wajibu wake. Mtoto wa Mungu anapoamua kusema, swali lake lisibaki kuwa, “Nitasemaje nisije nikamkasirisha mwenye mamlaka?” Ajiulize pia, “Nikinyamaza, ni nani ataendelea kuumia? Na nitakuwa mwaminifu kwa dhamiri yangu mbele za Mungu?” Hilo ndilo Kanisa tunalohitaji: lenye unyenyekevu wa kusikiliza, uadilifu wa kujisahihisha na ujasiri wa kusema kweli. Kanisa linaloomba kwa ajili ya watawala, linalowaonya wanapokosea, na linalosimama pamoja na wanaodhulumiwa. Kwa sababu wajibu wake wa kusema ukweli hauanzi pale Serikali inapouruhusu, wala hauishii pale Serikali inapochukizwa nao.
13
52
256
17,012
KIJIJI KINAUNGUA, VIONGOZI WANATEMBEA KWA MARINGO Rev. Peter Simon Msigwa Kinyonga anayetaka kupona kwenye kichaka kinachowaka moto lazima aache mwendo wa maringo aliourithi kwa mababu zake. Katika siasa, huu ni ujumbe kwa viongozi waliobweteka kwenye viti, wanaodhani kwamba kwa sababu jana mambo yalienda kwa namna fulani, hata kesho yataendelea hivyo hivyo. Nyakati zinabadilika. Mahitaji ya wananchi yanabadilika. Uvumilivu una mipaka. Huwezi kuongoza jamii inayokabiliwa na matatizo ya haraka kwa mazoea ya kuchelewesha maamuzi, kurudia ahadi na kuitisha kikao kingine kuhusu jambo ambalo wananchi wamelilalamikia kwa miaka. Mwananchi mwenye njaa hali ratiba ya vikao. Kijana asiye na ajira hawezi kuishi kwa makofi ya mkutano. Mgonjwa anayekosa dawa haponi kwa taarifa kwamba viongozi wameridhishwa na utekelezaji. Lakini kiongozi aliyebweteka anaweza kutazama hali hiyo yote na kusema: “Mambo yako sawa.” Yako sawa kwa nani? Kwa mwenye gari la serikali, mafuta ya serikali na matibabu yanayolipiwa? Au kwa mwananchi anayelazimika kuchagua kati ya kununua chakula na kununua dawa? Hatari ya madaraka ni kwamba yanaweza kumfanya kiongozi aishi mbali na matokeo ya maamuzi yake mwenyewe. Yeye anapochelewa kuchukua hatua, mwingine anakosa mlo. Anapoahirisha suluhisho, mwingine anafunga biashara. Anaposema “tutalifanyia kazi,” mwingine anapoteza matumaini. Utulivu wa ofisi yako si kipimo cha utulivu wa maisha ya wananchi. Na huu ni ujumbe pia kwa viongozi wa upinzani. Huwezi kutaka mabadiliko makubwa huku ukiendelea na maandalizi madogo, mipango isiyotekelezwa na migogoro ya nafasi. Huwezi kuwaita wananchi wasimame, wakati wewe mwenyewe umekaa kwenye faraja ya cheo chako. Uongozi unahitaji uwepo, maandalizi, nidhamu na uwajibikaji. Unahitaji kwenda kwa wananchi, kuwasikiliza, kuwaandaa kushiriki kwa amani na kuwaeleza kwa uwazi hatua zinazofuata. Hasira ya wananchi peke yake haiwezi kuchukua nafasi ya kazi ya uongozi. Kinyonga anatukumbusha kwamba kuna wakati mazoea huwa hatari. Kauli ya “hivi ndivyo tulivyozoea” haiwezi kuwa jibu wakati mazingira yamebadilika. Kubadili mwendo ni kuacha uzembe. Ni kuweka muda wa kutatua tatizo na kuwajibika ukishindwa. Ni kuacha kuwapima wasaidizi kwa wingi wa sifa wanazokupa na kuanza kuwapima kwa matokeo ya kazi zao. Ni kukubali kwamba anayekuonya anaweza kuwa anakusaidia kuliko anayekupigia makofi. Kiongozi anayekasirishwa zaidi na sauti ya malalamiko kuliko chanzo cha malalamiko hayo amepoteza dira ya wajibu wake. Viongozi, amkeni. Vyeo mlivyonavyo vina wajibu. Heshima mnayopewa ina matarajio. Muda mnaoutumia kujipongeza ni sehemu ya maisha ya wananchi ambayo haitarudi. Kichaka kinapowaka, kinyonga hakiokolewi na uzuri wa rangi yake, historia ya ukoo wake wala hadhi ya tawi alilokalia. Lazima atambue hatari na achukue hatua. Wananchi hawapaswi kulipia starehe ya viongozi waliobweteka. Badilisheni mwendo; timizeni wajibu.
14
73
7,626
Ninapomsikiliza Tundu Lissu akiendelea na hoja zake za mwisho, ninavutiwa na uwezo wake mkubwa wa kufikiri, kuchambua na kufafanua. Huyu mtu ana akili makini sana. Anaingia ndani ya kila hoja, anazingatia maelezo madogo na kuyaunganisha ili kuonesha picha pana. Kinachonigusa zaidi ni umakini wake: jambo ambalo msikilizaji anaweza kulipita, yeye analisimamia na kufafanua kwa nini lina maana. Hapo unaona tofauti kati ya kuzungumza kwa kujiamini na kuzungumza ukiwa umeelewa kwa kina unachokisema. Unaweza kutofautiana naye kisiasa, lakini uwezo wake wa kujenga hoja unastahili kutambuliwa. Akili yenye maandalizi, kumbukumbu na umakini hujidhihirisha katika maelezo.
37
152
975
39,911
Ukimya unakuwa usaliti pale ambapo kusema ni wajibu wa dhamiri, lakini tunachagua kulinda faraja yetu kuliko kutetea ukweli. Hutokea wakati ambapo: Tunashuhudia dhuluma, lakini tunanyamaza ili kulinda nafasi, vyeo au maslahi yetu. Tunaujua ukweli, lakini tunaacha uongo uharibu maisha na heshima ya mtu mwingine. Watu wanateseka chini ya uongozi wetu, lakini tunakataa kutambua maumivu yao. Tunakemea makosa ya wapinzani wetu, lakini tunatetea au kufumbia macho makosa yaleyale yanapofanywa na marafiki zetu. Wengine wanategemea sauti yetu kuwatetea, lakini tunawaacha kwa sababu kusema kunaweza kutugharimu. Si kila ukimya ni usaliti. Wakati mwingine mtu hunyamaza kwa ajili ya usalama, kutafakari, au kutafuta njia yenye busara ya kuchukua hatua. Lakini wajibu wa kusema huwa mkubwa zaidi kwa wale wenye mamlaka, ulinzi na uwezo wa kusaidia. Swali la kujiuliza ni hili: “Ukimya wangu unamlinda nani—na unamwacha nani bila ulinzi?” Ukimya wetu unapowalinda wenye nguvu huku ukiwatelekeza wanaoumia, unakoma kuwa kutopendelea upande wowote. Unakuwa ushirika katika dhuluma.
12
69
1,946
Uchawa hauwi elimu kwa sababu tu umefundishwa darasani Rev Peter Simon Msigwa Ukimwuliza mwanachama aliyepitia mafunzo ya chama chake: “Falsafa yenu ni nini? Itikadi yenu ni ipi? Mna mlengo gani? Sera zenu zinaeleza nini?” anabaki kukutajia majina ya viongozi na kurudia kaulimbiu. Hajui kutofautisha falsafa, itikadi, mlengo na sera. Lakini anajua nani wa kumsifia, nani wa kumshambulia na nani hapaswi kuulizwa maswali! Ukimwuliza tofauti kati ya nchi, taifa, dola na serikali, anavichanganya vyote na chama chake. Ndiyo maana kwake kukosoa serikali ni kuichukia nchi, kutofautiana na chama ni kukosa uzalendo, na kuhoji kiongozi ni kuwa adui wa taifa. Huu ni upungufu mkubwa wa elimu ya siasa wenye madhara kwa jamii. Nchi si mali ya chama. Serikali si nchi nzima. Dola haipaswi kuwa chombo cha viongozi wa chama. Na taifa lina watu wenye mitazamo tofauti ambao wote wana haki sawa ya kuwa sehemu yake. Hata tofauti ya Rais na Urais inakuwa tatizo! Rais ni mtu anayeshika nafasi kwa muda; Urais ni taasisi inayopaswa kuheshimiwa na kulindwa hata baada ya mtu huyo kuondoka. Kumwajibisha Rais kunalinda heshima ya Urais. Kumsifu hata anapokosea kunaidhoofisha. Sasa mafunzo yanaposhindwa kumfundisha mwanachama mambo haya ya msingi, lakini yakamjengea uwezo mkubwa wa kushangilia kila kauli na kutetea kila kosa, tunapaswa kuuliza: Humo mnafundisha nini hasa? Mnafundisha kujenga hoja au kuzima hoja? Kuheshimu kura au kushinda kwa gharama yoyote? Kuwatumikia wananchi au kuwaona wanaowapinga kama maadui wa kushughulikiwa? Mafunzo yenye maana yanapaswa kumwezesha mwanachama kukataa wizi wa kura, kupinga vurugu na kumwambia hata kiongozi wake: “Hapa umekosea.” Yakishindwa kumjengea ujasiri huo, yameacha pengo kubwa la maarifa na dhamiri. Mwanachama anayejua kumtetea kiongozi lakini hajui kutetea haki ya mwananchi amefundishwa utii bila kufundishwa wajibu. Na chama kinapozalisha watu wanaoweza kupiga makofi lakini hawawezi kuuliza maswali, kinajinyima uwezo wa kujisahihisha. Uchawa hauwi elimu kwa sababu tu umefundishwa darasani!
17
54
1,868
You can take away all my titles, but you can’t take away God’s favor upon my life.
7
19
248
3,207
MAFUNZO YA ITIKADI YANA FAIDA GANI KAMA HOJA ZINAJIBIWA NA POLISI? Rev Peter Simon Msigwa Mara kwa mara tunasikia Chama Cha Mapinduzi kikitangaza kwamba kimeendesha mafunzo ya itikadi na uenezi. Viongozi na vijana wake hupelekwa kwenye semina mbalimbali, wengine hadi China, wakidaiwa kwenda kujifunza uongozi, siasa, itikadi na namna ya kuimarisha chama. Lakini swali la msingi ni hili: Mafunzo hayo yana faida gani kama wahitimu wake hawawezi kusimama katika uwanja huru wa mawazo na kujibu hoja kwa hoja? Kama CHADEMA ikisema tunahitaji Katiba Mpya, jibu halipaswi kuwa polisi. CHADEMA ikihoji uhuru wa uchaguzi, jibu halipaswi kuwa kukataza mikutano. CHADEMA ikiuliza kuhusu haki, uwajibikaji na matumizi ya rasilimali za taifa, jibu halipaswi kuwa vitisho, kukamatwa au kufunguliwa kwa kesi. Hoja hujibiwa kwa hoja. Takwimu hujibiwa kwa takwimu. Sera mbadala hujibiwa kwa sera bora zaidi. Ukosoaji wa kisiasa hujibiwa kwa majadiliano ya kisiasa—si kwa nguvu ya dola. Chama chenye itikadi imara hakihitaji polisi kukitetea dhidi ya maneno. Kinahitaji viongozi wenye maarifa, ujasiri na uwezo wa kuwashawishi wananchi. Kama baada ya mafunzo yote, ziara zote na safari zote za China bado chama kinahitaji polisi, vyombo vya usalama na vizuizi vya mikutano ili kukabiliana na wapinzani wake, basi kuna uwezekano wa mambo mawili: ama mafunzo hayo hayana maudhui yanayojenga uwezo wa kufikiri na kujenga hoja, au madhumuni yake si kuelimisha bali kuwafundisha wanachama kutii mamlaka bila kuuliza maswali. Mafunzo ya kweli ya itikadi yanapaswa kumwezesha mwanachama kueleza: Kwa nini chama chake bado kinastahili kuongoza? Kina majibu gani kwa matatizo ya wananchi? Kinawezaje kutetea rekodi yake bila vitisho? Kina sera gani bora kuliko za wapinzani? Kwa nini wananchi wakiamini kwa hiari bila kushurutishwa? Kama mwanachama hawezi kujibu maswali hayo, lakini anaweza kupiga makofi, kuimba nyimbo za sifa na kuwashambulia wakosoaji, huyo hajafundishwa itikadi amefundishwa utii. Na kama vijana wanasafiri hadi China kujifunza siasa, lakini wanaporudi hawawezi kukaa mezani na vijana wa CHADEMA katika mdahalo wa wazi, basi hizo safari zinakuwa utalii wa kisiasa unaolipiwa kwa jina la mafunzo. CCM ijiulize kwa uaminifu: Kwa nini chama chenye historia ndefu, rasilimali nyingi, wataalamu wengi na mafunzo yasiyokwisha kinashindwa kuvumilia hoja za chama cha upinzani bila msaada wa vyombo vya dola? Udhaifu wa hoja hauwezi kufichwa milele kwa nguvu ya polisi. Unaweza kuzuia mkutano, lakini huwezi kuzuia swali. Unaweza kumkamata msemaji, lakini huwezi kuifunga hoja. Unaweza kunyamazisha sauti kwa muda, lakini huwezi kuamuru dhamiri za wananchi zikae kimya. Polisi akitumika kujibu hoja ambayo mwanasiasa ameshindwa kuijibu, hapo polisi hajathibitisha nguvu ya chama amefichua udhaifu wake. Chama kinachojiamini kifungue uwanja wa kisiasa. Kiruhusu mikutano. Kikubali midahalo ya wazi. Kiwalete vijana wake waliopata mafunzo wakutane na vijana wa CHADEMA. Wananchi wasikilize pande zote, wapime hoja, halafu waamue. Kwa sababu katika demokrasia, chama hakithibitishi ubora wake kwa uwezo wa kuwakamata wapinzani. Kinathibitisha ubora wake kwa uwezo wa kuwashinda kwa hoja, sera na kura huru za wananchi. Kwa hiyo, msituambie tu mmeendesha mafunzo ya itikadi. Tuonyesheni matokeo yake. Tuonyesheni viongozi wanaoweza kujibu hoja bila hasira, kujenga hoja bila matusi, na kushindana bila kuitisha polisi. Mafunzo yasiyozalisha fikra huru yanazalisha wafuasi, si viongozi. Itikadi inayolindwa kwa virungu badala ya hoja si itikadi yenye nguvu ni hofu iliyovaa sare ya mamlaka.
2
13
69
19,940
SERIKALI HAIPASWI KUTULAZIMISHA KUCHAGUA KATI YA MAENDELEO NA HAKI Rev Peter Simon Msigwa Ujenzi wa barabara, madaraja, madarasa na vituo vya afya ni muhimu lakini hauwezi kuwa mbadala wa haki, ukweli na utu wa mwanadamu. Barabara nzuri haiwezi kufunika damu ya wasio na hatia. Daraja haliwezi kutuunganisha ikiwa dhuluma imetutenganisha. Darasa haliwezi kuitwa maendeleo ikiwa wanafunzi wanafundishwa kunyamaza mbele ya uovu. Na kituo cha afya hakiwezi kuliponya taifa ambalo dhamiri yake imejeruhiwa. Serikali haipaswi kutulazimisha kuchagua kati ya maendeleo na haki. Wananchi wanastahili vyote: barabara nzuri na uhuru wao; hospitali bora na haki zao; madarasa mapya na uchaguzi wa haki; maji safi na utawala unaowajibika. Fedha zinazojenga miundombinu ni kodi za wananchi. Kwa hiyo, ujenzi huo si zawadi ya watawala wala hisani ya chama tawala ni wajibu wa serikali kwa wananchi wake. Serikali haiwezi kutumia wajibu mmoja kuficha kushindwa kwake katika wajibu mwingine. Huwezi kujenga daraja mchana, halafu usiku ukabomoa haki. Huwezi kufungua darasa jipya, halafu ukafunga midomo ya wanaouliza maswali. Huwezi kujenga kituo cha afya, halafu ukavunja mioyo ya familia zinazodai kujua wapendwa wao waliotekwa, kujeruhiwa au kuuawa. Huwezi kujenga barabara nzuri kuelekea kwenye taifa lisilo na haki na kuiita hiyo maendeleo. Maendeleo ya kweli hayapimwi kwa urefu wa lami pekee, bali pia kwa kiwango cha uhuru wa wananchi. Hayapimwi kwa idadi ya majengo yaliyosimamishwa pekee, bali kwa usalama wa watu, uhuru wa mahakama, uwajibikaji wa viongozi na heshima kwa uhai wa binadamu. Kwa hiyo, ukweli unaposhambuliwa, utu unapokanyagwa na wasio na hatia wanapoonewa, tusinyamazishwe kwa kutajiwa miradi ya maendeleo. Hatuli lami. Hatuishi ndani ya madaraja. Tunahitaji taifa ambalo barabara zinajengwa, lakini pia haki inatendeka; madarasa yanaongezeka, lakini pia ukweli unafundishwa; vituo vya afya vinafunguliwa, lakini pia uhai wa kila mwananchi unalindwa. Kwa sababu taifa linaweza kuwa na majengo marefu lakini likawa limeporomoka kimaadili. Linaweza kuwa na barabara nyingi lakini likawa limepoteza njia. Linaweza kuwa na madaraja makubwa lakini likashindwa kujenga daraja kati ya mamlaka na wananchi. Maendeleo yasiyo na haki ni mapambo juu ya jeraha. Maendeleo yasiyo na uhuru ni gereza lililopakwa rangi. Na maendeleo yanayotumiwa kuficha dhuluma si maendeleo ni propaganda.
3
33
100
2,044
HAKUNA KITU CHA KUDUMU KATIKA DUNIA HII Rev Peter simon Msigwa Hakuna kitu cha kudumu katika dunia hiisi maumivu, si furaha, si utajiri, si umaskini, si umaarufu, si madaraka, wala si nafasi uliyonayo leo. Maisha hubadilika. Majira hubadilika. Watu hubadilika. Mazingira hubadilika. Aliye juu leo anaweza kuwa chini kesho; na aliyepuuzwa leo anaweza kuwa mtu anayehitajika zaidi kesho. Ndiyo maana tusitafsiri hali ya sasa kana kwamba ndiyo hukumu ya mwisho ya maisha yetu. Unapopita katika maumivu, usikate tamaa. Maumivu yanaweza kuwa makali, lakini hayana mamlaka ya kuamua mwisho wa maisha yako. Usiku unaweza kuwa mrefu, lakini haujawahi kuzuia asubuhi kufika. Machozi yanaweza kudumu kwa muda, lakini hayawezi kuzuia furaha kurudi. Unapofanikiwa, usiwe na kiburi. Kiti unachokalia leo kilikaliwa na mwingine kabla yako, na siku moja kitakaliwa na mwingine baada yako. Cheo ni cha muda; mamlaka ni dhamana; umaarufu ni upepo. Wanaokushangilia leo wanaweza kukusahau kesho. Kwa hiyo, usiwadharau watu kwa sababu tu leo una nguvu kuliko wao. Katika siasa, somo hili ni kubwa zaidi. Serikali hubadilika. Vyama hubadilika. Watawala huondoka. Magereza hufunguka. Wafungwa wa kisiasa wanaweza kuwa viongozi wa taifa, na wale waliowafunga wakabaki wakijitetea mbele ya historia. Mtu anaweza kuwa na jeshi, polisi, mahakama na vyombo vya habari upande wake, lakini bado asiwe na uwezo wa kuzuia wakati. Madaraka yanaweza kuchelewesha mabadiliko, lakini hayawezi kuyazuia milele. Historia imejaa watawala waliodhani wataendelea kutawala daima. Walijenga sanamu zao, wakafuta majina ya wapinzani wao na kuwafunga waliowakosoa. Lakini leo sanamu zao zimeanguka, majina yao yanatajwa kwa aibu, na waliowatesa wanakumbukwa kama mashujaa. Ndiyo maana ukiwa madarakani, tawala kwa haki. Usitumie nafasi ya muda kutengeneza majeraha ya kudumu. Usimdhalilishe mtu kwa sababu leo hana uwezo wa kujitetea. Usitumie taasisi za taifa kuwaadhibu wale wasiokubaliana nawe. Meza za kisiasa hugeuka. Siku moja unaweza kuhitaji haki ileile ambayo leo unawanyima wengine. Na ukiwa umeanguka, umepuuzwa au umefungwa usione kana kwamba kila kitu kimekwisha. Gereza la leo linaweza kuwa darasa la kiongozi wa kesho. Kukataliwa kwa leo kunaweza kuwa maandalizi ya kukubalika kesho. Yusufu alikuwa mfungwa kabla hajawa mtawala. Mandela alikuwa gerezani kabla hajawa rais. Hali ya sasa si lazima iwe utambulisho wako wa milele. Kwa hiyo: Ukiwa juu, kuwa mnyenyekevu. Ukiwa chini, kuwa na matumaini. Ukiwa na nguvu, tenda haki. Ukiwa dhaifu, usikate tamaa. Ukipongezwa, usijione mungu. Ukikataliwa, usijione huna thamani. Mwisho wa yote, cheo kitaondoka, mali itaachwa, nguvu zitapungua na makofi yatanyamaza. Kitakachobaki si ukubwa wa nafasi uliyokuwa nayo, bali namna ulivyowatendea watu wakati nafasi hiyo ilikuwa mikononi mwako. Hakuna kitu cha kudumu katika dunia hii. Kwa hiyo, usijivune sana katika ushindi wako, wala usikate tamaa sana katika kushindwa kwako. Maisha yana tabia ya ajabu ya kugeuza meza mfungwa wa leo anaweza kuwa rais wa kesho, na mtawala wa leo anaweza kuwa mshtakiwa wa historia.
4
34
137
3,933