#TANZANIA: THRDC YATAKA WAFANYAKAZI WA PWC WALIOZUIWA ARUSHA KUACHIWA
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) leo Oktoba 07, 2026 umeeleza kusikitishwa na kukamatwa kwa wafanyakazi watatu wa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na THRDC, wafanyakazi hao walikamatwa na Polisi Oktoba 06, 2026. Waliotajwa ni Thadeus Clamian, Nangei Meitaya na Ezekiel Kishau, pamoja na Salangat Makko, ambaye kwa mujibu wa taarifa hiyo si mfanyakazi wa PWC.
THRDC imesema taarifa ilizopokea zinaeleza kuwa waliokamatwa wanatuhumiwa kupanga maandamano kwa ajili ya wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Aidha, shirika hilo limesema limepokea taarifa kwamba Polisi wameendelea kuwatafuta wafanyakazi wengine wa PWC, huku baadhi yao wakidaiwa kufuatiliwa hadi majumbani mwao nyakati mbalimbali wakati mwingine wanafuatiliwa hadi nyakati za usiku.
Taarifa hiyo pia inasema kuwa Oktoba 05, 2026 Polisi walifanya upekuzi katika moja ya makazi ya mfanyakazi wa PWC wakati wa usiku, bila kueleza sababu za upekuzi huo, jambo ambalo THRDC imesema limeongeza hofu na wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa PWC, familia zao na mashirika jijini Arusha.
Pia, THRDC imesema imewaelekeza Mawakili Simon Mbwambo na Ally Mhyellah kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Kati, Arusha kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa waliokamatwa.
Kwa upande mwingine, Wakili Lairumbe anaendelea kufuatilia suala hilo kwa niaba ya PWC.
Aidha, THRDC imezitaka mamlaka za Polisi kuwaachia wafanyakazi hao bila masharti, ikidai kuwa hakuna shirika mwanachama wa mtandao huo linaloratibu maandamano.
Pia, imeitaka Polisi kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote waliokamatwa wanapewa fursa ya kuwasiliana na Mawakili pamoja na familia zao.
Taarifa hiyo imetolewa na Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC.