Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimezindua rasmi ofisi zake mpya na za kisasa za mapokezi zilizopo katika jengo la MPL, ikiwa ni sehemu ya jitihada endelevu za kuboresha huduma kwa wanafunzi, wageni, na watumishi wa chuo.
Ofisi hizo mpya zimebuniwa kuwa kitovu cha huduma kwa wageni wanaotembelea chuo kwa mara ya kwanza, zikiwa na jukumu la kutoa taarifa, kutoa maelekezo, na kuratibu huduma mbalimbali za msingi kwa wageni na wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kuanzishwa kwa ofisi hizo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa MUHAS wa kuboresha utoaji huduma kwa jamii na kuhakikisha chuo kinaendelea kuwa mfano wa ubora katika huduma zake.
“Tunataka kila anayefika MUHAS apokee huduma kwa weledi na kwa wakati. Ofisi hizi ni sehemu ya dhamira yetu ya kutoa huduma bora zinazokwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia,” alisema Prof. Kamuhabwa.
Jengo la MPL, ambalo linamilikiwa na MUHAS, linatumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo ofisi, ukumbi wa mikutano, na sasa limeongezewa huduma ya mapokezi yenye hadhi ya kisasa.
Ofisi hizo zimejengwa kwa muundo wa kisasa na zimewekewa mifumo ya TEHAMA, mawasiliano, na uhifadhi wa kumbukumbu, ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi, weledi, na kwa wakati. Ofisi zitakuwa wazi katika saa zote za kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanafunzi, wageni, na wadau wa MUHAS.
Viongozi mbalimbali wa chuo, wakuu wa idara, pamoja na watumishi walihudhuria hafla hiyo fupi ya uzinduzi iliyoambatana na pongezi kwa uongozi wa MUHAS kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma chuoni.