Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Asemewe, Geofrey Kiliba, amesema aliwahi kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan amruhusu kujibu matusi ya wanasiasa wa upinzani kwa lugha kama wanayotumia dhidi yake, lakini Rais alimkataza na alimshauri badala yake kutumia elimu na kueleza kazi zinazofanywa na Serikali.
Kiliba ameyasema hayo leo, Oktoba 20, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisimulia tukio la siku aliyopata fursa ya kukutana na Rais Samia katika mkutano uliohusu changamoto za vyuo na vyuo vikuu nchini.
Amesema alipata nafasi ya kuzungumza na Rais pembeni ya mkutano huo na kumweleza namna anavyoumia anapoona kile alichokitaja kuwa ni juhudi za baadhi ya wanasiasa wa upinzani kupotosha umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kumshambulia Rais kwa lugha zisizofaa.
“Nilimwambia Mheshimiwa Rais kwamba ninaumia sana kwa kazi kubwa unayoifanya ndani ya nchi yetu kwenye miundombinu, afya, elimu na maji, lakini ninaumia ninavyoona wanasiasa, hasa kutoka upinzani, wanavyolaghai umma na kuongea kana kwamba hakuna kilichofanyika, wanafika mbali na kuanza kukutukana,” amesema Kiliba.
Ameeleza kuwa katika mazungumzo hayo alimuuliza Rais kwa nini anaendelea kukaa kimya licha ya mashambulizi hayo, huku akimuomba amruhusu na yeye kuwajibu wanasiasa hao kwa lugha wanazotumia, akiamini kuwa kufanya hivyo kungekuwa njia ya kukabiliana nao.
Hata hivyo, Kiliba amesema Rais Samia alimshauri kutotumia matusi kujibu matusi, bali kuelekeza nguvu katika kuwaelimisha wananchi kuhusu shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali. Kwa mujibu wa Kiliba, Rais alimweleza kuwa hata inapowezekana, ni vyema kuwachukua wanaopinga na kuwaonyesha miradi inayotekelezwa ili wajionee wenyewe.
Kiliba amesema ushauri huo unaonyesha msimamo wa Rais Samia kuhusu namna ya kukabiliana na ukosoaji wa kisiasa, akisisitiza kuwa badala ya kutumia nguvu au lugha za matusi, ni muhimu kutumia hoja, elimu na ushahidi wa kazi zinazofanyika nchini kujibu wakosoaji.