Mkutano wangu na waandishi wa habari niliokuwa nifanye katika Hotel ya Golden Tulip nimeuahirisha.
Nimesikiliza hotuba za Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Wameeleza vizuri kuhusu uvumi na upotoshaji uliokuwa ukifanyika juu yangu na misimamo juu ya chama chetu.
Nimedumu katika mapambano haya kwa zaidi ya miaka 22. Nimeenda lock-up zaidi ya mara 50. Nimezunguka nchi hii usiku na zaidi ya mara tatu. Nimewahi kuwa magerezani mara kadhaa, nimekoswa kuuawa zaidi ya mara tatu, na nimewahi kukimbia nchi.
Katika yote haya, nimekuwa nikitoa sadaka kubwa kwa ajili ya mapambano haya, ikiwemo ku-sacrifice familia yangu mara zote.
Kazi hii kwangu si ajira, si cheo, wala si njia ya kujitafutia maslahi. Ni huduma. Ni wito. Ni kama injili ninayoamini na kuitumikia.
Kwa hiyo, siwezi kuruhusu uvumi, upotoshaji au tafsiri za watu kuniondoa kwenye misingi ambayo nimeisimamia kwa zaidi ya miongo miwili.
Nitakuwa kwenye mapambano haya kwa imani, ujasiri na dhamira njema siku zote.