Safi๐
VIDEO:
Wachimbaji wadogo wa madini ya nickel katika Kijiji cha Nditi wilayani Nachingwea mkoani Lindi kupitia Umoja wa Vikundi vya Wachimbaji wa Madini, wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto ya utendaji wa wawezeshaji wanaofanya shughuli za uchimbaji katika maeneo yao ya leseni.
Mwenyekiti wa UVIWAMA, Abdallah Matayo Nkane amesema baada ya chama hicho kupewa leseni Julai mwaka jana, walipata wawezeshaji wanne katika maeneo manne ya leseni, lakini utendaji wao umekuwa wa kusuasua tangu Oktoba mwaka huo, hali iliyosababisha wanachama kutonufaika na shughuli za uchimbaji na mapato ya Serikali kutopatikana kwa kiwango kinachotarajiwa.
Nkane amesema awali chama hicho kilikuwa na mwekezaji mwingine, lakini baada ya Serikali kuelekeza watafute mwekezaji wa ndani, walipata wawezeshaji hao ambao, kwa mujibu wa chama, hawajawa na uwezo wa kutosha kifedha na kiteknolojia.
Mchimbaji mdogo wa nickel na mwanachama wa UVIWAMA, Said Mkindiga, amesema wawezeshaji waliopo wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji, fedha na vifaa, hali inayosababisha uchimbaji kufanyika kwa kasi ndogo na kwa mbinu zisizokuwa na tija.
Naye mkazi wa Nditi, Atia Ali Chitumbi, amesema hali hiyo imeathiri uchumi wa wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea mgodi huo kupata kipato cha kuendesha familia, kusomesha watoto na kukidhi mahitaji ya kila siku.
Kwa upande wake, Ismael Ndoro, mwanachama na mjumbe wa Bodi ya UVIWAMA, amesema wanachama wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa kipato kutokana na uzalishaji mdogo.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo amesema tatizo kubwa ni kukosekana kwa mkataba kati ya wanakikundi na wawezeshaji ili kuweka makubaliano ya kazi.
Aidha, Moyo amewatupia lawama viongozi wa kikundi hicho kwa kutokuwa wakweli kwa wanachama wao hali iliyosababisha kuwa na mgogoro usiokwisha na wawezeshaji wao.